Mabingwa watetezi, Yanga wanashika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi tatu baada ya kucheza mchezo mmoja, lakini ikiwa na michezo miwili mkononi dhidi ya Ndanda kesho, kisha Jumamosi itacheza na Majimaji kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Pluijm amesema wanatakiwa kushinda michezo hiyo ili wakae sawa kiakili kwani kushinda mechi moja pekee bado hawawezi kujisifu ukizingatia wao ndiyo mabingwa watetezi.
“Tunaendelea na maandalzi kwa ajili ya mchezo ujao dhidi ya Ndanda, tunatakiwa kushinda ili kujiweka sawa katika ligi.
“Tutakuwa na kazi kubwa msimu huu kutetea ubingwa kwani kila timu inatutolea macho na tunakamiwa kwa sababu kila mpinzani wako anataka pointi dhidi yako.
“Licha ya kwamba hatujapumzika tangu kumalizika kwa ligi ya msimu uliopita na wachezaji wengi watakuwa wamechoka, lakini hilo halinipi shida kwa sababu nina kikosi kipana kitakachoweza kunipa matokeo mazuri msimu huu,” alisema Pluijm.
Kocha wa Ndanda, Mawazo amesema baada ya kupoteza michezo miwili mfululizo hawatakubali kuwaachia Yanga pointi.
Ndanda imepoteza michezo miwili tangu kuanza kwa ligi msimu huu dhidi ya Simba na Mtibwa Sugar, hivyo kuwa timu ya pili kutoka mkiani ikiwa haina pointi, jambo ambalo linamuumiza Mawazo.
Kocha huyo alisema lazima wachezaji wake wapambane katika mchezo huo ili kupata pointi hata moja kuliko kufungwa tena mchezo wa tatu mfululizo.
“Hadi sasa sisi na Majimaji ndiyo hatuna pointi katika timu zote zinazoshiriki ligi, tumekuwa tukipambana lakini bahati mbaya tumepoteza michezo yote miwili tuliyocheza.
Maoni
Chapisha Maoni