Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema mkono wa serikali kisheria ni mrefu, hivyo wazazi au walezi watakaokwenda kinyume watahakikisha kuwa wanakamatwa na kufikishwa mahakamani. Ummy ameyasema hayo jana katika tamko maalumu alilolitoa kwa wanafunzi hao waliohitimu elimu ya msingi nchini kote.
Alisema wazazi na walezi wanapaswa kutambua umuhimu wa mtoto wake kuendelea kielimu, na kukua kimwili na kiakili kabla ya kuingia katika ndoa kwani elimu ya watoto wa kike ni moja ya njia bora za kupunguza umaskini katika mataifa yanayostawi.
“Natoa rai kwa wananchi wote kuendelea kutoa taarifa kwa mamlaka husika za Serikali za Mtaa, Kijiji, Kata, Wilaya na hata katika Madawati ya Jinsia na Watoto yaliyopo Polisi, pale watakapobaini mzazi au mlezi au taasisi anaenda kinyume na jitihada za serikali za kumuendeleza mtoto kielimu hasa katika kudhibiti ndoa za watoto waliomaliza Elimu ya Msingi hususan katika kipindi hiki cha kusubiri matokeo yao,” alisema Ummy.
Aidha, amewataka wahitimu wa darasa la saba waliomaliza mitihani yao juzi, kutojihusisha na tabia au vitendo vyovyote vinavyohatarisha afya, usalama na maendeleo yao.
Takwimu zinaonesha kuwa wanafunzi 795,761 (wavulana 372,883 sawa na asilimia 46.86 na wasichana 422,878 sawa na asilimia 53.14) walisajiliwa na kufanya mtihani wa darasa la saba mwaka huu.
“Hivyo ningependa kutumia fursa hii kuwaasa watoto waliomaliza darasa la saba kutojihusisha na tabia au vitendo vyovyote vinavyohatarisha afya, usalama na maendeleo yao, kama vile kujihusisha kwenye masuala ya ngono, matumizi ya dawa za kulevya na vileo katika kipindi hiki cha kusubiri matokeo ya mitihani yao,” alisema Ummy.
Alisema watoto wa kike na kiume wajitambue, na wajue kuwa wao ni hazina ya pekee katika maendeleo ya nchi yetu. Kipindi hiki wakitumie vizuri kwa kuwa waadilifu, waaminifu, wenye bidii na kuzingatia kanuni za nidhamu na tabia njema huku wakijiandaa kwa ajili ya kuendelea na elimu ya sekondari.
Ummy alisema serikali imekusudia kumpa kila mtoto nafasi ya kupata elimu ya sekondari na tayari msingi umeshawekwa na Rais wa Awamu ya tano, Dk John Magufuli wa kutoa elimu ya sekondari bure hivyo hawatafurahi kuona mmoja kati ya watoto hao waliomaliza elimu ya msingi juzi anaikosa nafasi hiyo kwa sababu zinazoweza kuzuilika.
“Nawaasa watoto wote kutumia kipindi hiki kwa kukataa kurubuniwa, kushawishiwa na kujiingiza katika mambo yenye kuhatarisha afya, usalama na maendeleo yao,” alisema Ummy.
Maoni
Chapisha Maoni