Nape aliyasema hayo wakati akizungumzia utekelezaji wa mipango na mikakati ya wizara yake katika kipindi cha ‘Tunatekeleza’ kinachorushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1).
“Tunatarajia kwamba Bunge hili linaloanza Septemba 6 (leo), tunaweza kuupeleka Muswada huu bungeni ukasomwa kwa mara ya kwanza, na Bunge la Novemba tukaanza mjadala wake na nina matumaini kwamba huu mwaka wa fedha hautaisha kabla hatujapitisha muswada huo,” alisema.
Alisema; “Muswada umefikia mahali pazuri na tumeukamilisha sasa tupo tayari kufuata taratibu za kawaida za kuufikisha bungeni na kusomwa kwa mara ya kwanza na ni muswada ambao ni mzuri, utaondoa kelele nyingi ambazo zimekuwa zikizungumzwa, tumekuwa na Sheria tangu mwaka 1976 ambazo zimekuwa zikilalamikiwa.”
Alisema muswada huo unatarajiwa kuondoa sheria kandamizi na kutengeneza mazingira mazuri ya ukuaji wa tasnia ya habari na kwamba si sheria ambayo itatetea mambo yasiyofaa.
Aidha alisema, bado kuna fursa ya wadau kuendelea kutoa maoni yao baada ya kupelekwa bungeni, na kuwa muswada huo umetolewa maoni mengi ya wadau ikilinganishwa na miswada mingine.
“Tunataka muswada huu uwafikie wadau wote na watoe maoni yao na maoni yote tutayapitia na kuyafanyia kazi... Ukishasomwa bungeni utapewa Kamati ya Bunge na itatafuta maoni ya wadau ili sheria hii isiwe ni ya serikali bali tunataka iwe ya wadau ili tasnia hii iendelee kukua zaidi.”
Akizungumzia maudhui ya vipindi katika baadhi ya vipindi alisema kuwa muswada unaokuja umeunda kamati ambazo pia zitasimamia hadi ubora wa elimu inayotolewa kwenye tasnia ya habari. “Tunataka mwandishi wa habari angalau awe na Shahada.... waandishi wengi wanapenda siasa maana haifikirishi, tunataka waandishi wawe na ubobezi. Tunapendekeza katika muswada pia, uwepo mfuko wa kusaidia taaluma ya waandishi wa habari,” alisema.
Alisema kuhusu adhabu ya kufungiwa vyombo vya habari inabidi iangaliwe sheria upya ili idhibiti na kushughulika na mwandishi badala ya kukiadhibu chombo cha habari na kukosesha mamia ya watu kazi kutokana na kosa la mtu mmoja.
Aidha aliwataka maofisa habari wa taasisi za umma kutoa habari kwa wakati kwa kuwa Watanzania wana haki ya kupatiwa habari kwa wakati.
“Nimegundua uwezo wa baadhi ya maofisa habari ni mdogo, hivyo tunaanza kwa kuboresha vitengo vyetu vya habari...pia sheria itawabana watendaji wa umma kuhakikisha wanawaruhusu maofisa habari wao kuingia katika vikao vya maamuzi ili wajue yanayoendelea,” alisema.
Aidha alisema wakipata taarifa ya ofisa habari anayekumbatia habari inayotakiwa kwenda kwa umma wataelekeza mamlaka inayohusika imuondoe kwa kuwa hafai.
Alisema pia wataboresha Idara ya Habari (MAELEZO) ili iwe ni ya kisasa zaidi ili iweze kuyafikia maeneo mengi ya vijijini sambamba na kuimarisha maslahi ya wafanyakazi wake.
Maoni
Chapisha Maoni