Shirikisho la mifuko ya hifadhi ya jamii Tanzania (TSSA) limeazimia kujenga viwanda vitakavyoajiri zaidi ya asilimia 40 ya watanzania na limeitaka serikali kuboresha mitaala kwenye vyuo vikuu na vyuo vya ufundi ili kupata wataalam watakaovihudumia.
Shirikisho hilo limesema litajenga viwanda vikubwa, vya kati na vidogo vitakavyotumia malighafi zinazozalishwa nchini ili kupanua wigo wa ajira kwa watanzania.
Katibu mkuu wa shirikisho hilo, Meshack Bandawe amesema baadhi ya viwanda hivyo vitajengwa na mashirika hayo na vingine vitajengwa na shirika moja moja kulingana na maeneo na upatikanaji wa rasilimali na kipaumbele kitatolewa kwa viwanda vya nguo, sukari, vipuri, chai na madawa.
Kabla ya shirikisho hilo kutangaza azma hiyo ya kujenga viwanda, shirikisho hilo lilikutana na mawaziri wa wizara za viwanda, biashara na uwekezaji,kilimo,mifugo na uvuvi, ofisi ya waziri mkuu, sera, bunge,vijana, ajira na walemavu, afya na maendeleo ya jamii,wanawake wazee na watoto, ofisi ya rais tawala za mikoa na serikali za mitaa ambazo baadhi ya mawaziri wake wameridhia mpango huo.
Uamuzi huo umechukuliwa kufuatia ushauri wa Rais Dkt John Pombe Magufuli kwa mashiriki ya hifadhi ya jamii kuwa yanapaswa kuanza kuwekeza kwenye ujenzi wa viwanda na sio kujenga majengo pekee ambayo hayawanufaishi wananchi wa kawaida.
Maoni
Chapisha Maoni