Facebook imebatilisha uamuzi wake wa awali wa kufuta moja ya picha mashuhuri ya wakati wa vita vya Vietnam.
Picha
hiyo inamuonyesha mtoto msichana aliyekuwa bila nguo akikimbia moto
katika kijiji kimoja, katika shambulizi lililotekelezwa kwa kutumia
kemikali ya napalm.Facebook ilifuta picha hiyo kwa misingi kwamba ilikuwa ya uchi.
Facebook inasema imerejesha picha hiyo kutokana na umuhimu wake wa kihistoria.
Gazeti moja nchini Norway, Aftenposten, liliongoza shutuma dhidi ya Facebook, baada ya kampuni hiyo kufunga akaunti ya mmoja wa wanahabari wake, aliyetumia picha hiyo.
Mhariri wa gazeti la Afte-posten la Norway, amesema uamuzi wa Facebook kufuta picha hiyo inaonyesha wazi haiwezi kutofautisha kati ya picha za ponografia na zile zinazohusiana na historia ya matukio muhumu duniani.
Waziri mkuu wa Norway ambaye awali alichapisha picha hiyo kwenye akaunti yake kama ishara ya maandamano, amekaribisha uamuzi wa Facebook wa kurejesha picha hiyo.
"wamefanya vizuri sana, mimi ni waziri mkuu aliye na furaha, inaonyesha kwamba matumizi ya mitandao ya kijamii yanaweza kuleta mabadiliko ya kisiasa, hata kwa mitandao ya kijamii yenyewe" Waziri mkuu Erna Solberg ameiambia BBC.
Msichana huyo ni nani?
Kim Phuc, alikuwa mwenye umri wa miaka 9 wakati picha hiyo ilipochukuliwa, akikimbia kuokoa maisha yake, baada ya shambulizi la Napalm, kaskazini mwa Saigon mwezi Juni 1972.Alikumbwa na majeraha mabaya ya moto.
Mpiga picha Nick Ut na mwanahabari wa ITN Christopher Wain walimpeleka hospitalini.
Waliambiwa kwamba hakukuwa na matumaini kwamba msichana huyo angeendelea kuishi.
Baada ya kulazwa hospitalini kwa kipindi cha miezi 14, na kufanyiwa upasuaji mara 17 , aliruhusiwa kuenda nyumbani.
Maoni
Chapisha Maoni