Arusha. Mbunge wa Simanjiro (Chadema), James Ole Milya amesema hatua ya Naibu Spika, Dk Tulia Ackson kumsimamisha kuhudhuria vikao vya Bunge ni kutokana na chuki binafsi dhidi yake.
Amedai kuwa Dk Tulia alianza kumchukia toka alipopeleka hoja ya kutaka kumg’oa bungeni.
Pia, amedai pamoja na kusimamishwa, lakini Serikali haijajibu hoja yake ya msingi hadi sasa aliyotaka kujua hatima ya kufukuzwa kazi kwa zaidi ya wafanyakazi 200 wa Kampuni ya Mgodi ya Tanzanite One katika mazingira ya kutatanisha na kutaka mkataba wa kampuni hiyo uchunguzwe kwa kina.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili jana jijini Arusha, Ole Milya alisema alitegemea kuna siku Naibu Spika huyo angemtimua, hivyo alishajiandaa kisaikolojia.
Hata hivyo, alisisitiza Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge haikumtendea haki baada ya kukataa kupokea ushahidi wake kuthibitisha uhusiano wa mmoja wa wabia wa kampuni hiyo na Waziri Jenister Mhagama.
Ole Milya ambaye amesimamishwa kuhudhuria vikao vitano vya Bunge kwa kuliambia uongo kuwa mmoja wa wabia wa kampuni ya Sky Associates inayomiliki na mgodi wa Tanzanite One unaodaiwa kunyanyasa wananchi ni shemeji ya Waziri Mhagama.
Lakini, Dk Tulia alisema Mhagama katika maelezo yake alieleza kwamba mtu huyo si shemeji yake na kuwasilisha malalamiko kwa kamati hiyo na baada ya kuchunguza, Ole Milya alishindwa kuthibitisha.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, George Mkuchika alipotakiwa kuzungumzia suala hilo alisema yeye ni hakimu na utaratibu haumruhusu kuzungumza chochote baada ya kutoa uamuzi ukatangazwe kwenye vyombo vya habari.
“Nikishatangaza uamuzi sipaswi kwenda kwenye magazeti, utaratibu hauko hivyo, siwezi kutangaza uamuzi halafu nikaenda kwenye magazeti kuzungumza tena,” alisema Mkuchika.
Akizungumzia kuhusu wafanyakazi hao, Ole Milya alisema kitendo cha kufukuzwa kazi kimesababisha waendelee kuhangaika mitaani kudai haki zao.
Alisema mamlaka zinapaswa kuchunguza mkataba wauendeshaji wa kampuni hiyo kwa kuwa pamoja na wazawa kupewa dhamana ya kuendesha, imeshindwa kuleta manufaa kwa wakazi wanaouzunguka mgodi huo. “Tanzanite One wachunguzwe wamepataje mkataba? watumishi 200 wamefukuzwa kinyemela, kampuni wamepewa wazawa lakini haiwasadii wakazi wa Simanjiro na Serikali iko kimya,” alisema.
Maoni
Chapisha Maoni